MFULULIZO: AGANO LA UTAKASO.
SOMO: MWANZO 1:26-28.
Utawala na mamlaka ndiyo Agano la urithi wetu katika Yesu Kristo. Kupitia utakaso tumepewa nguvu na uwezo wa kutawala katika maisha, kutawala juu ya dhambi, utumwa, unyanyaso na nguvu zote za shetani. “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini na ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi”-Mwanzo 1:28.
Utawala ndio mpango wa Mungu kwa mwanadamu tangu kuumbwa. Mungu aliumba mwanadamu kwa chapa na mfano wake.
Mungu hakumuumba mwanadamu aweze kunyanyaswa na hali yoyote au kuimbe chochote.
Mungu alimuumba mwanadamu kuwa mtawala, akampa mamlaka yote kudhibiti viumbe vingine vyote.
Mungu alimpa mwanadamu kumiliki, kutawala na kuwa na mamlaka juu ya kazi ya mikono yake.
Utawala na mamlaka hayo yote yalitolewa na Mungu kwa uhuru wake kuwa baraka juu ya mwanadamu.
Lakini, dhambi ilipoingia duniani yale mamlaka na utawala aliyopewa mwanadamu yaligeuka yakawa hofu, utumwa na kushindwa.
Lakini sasa katika Yesu Kristo, ukombozi wake umerejesha Wakristo kwa mahali pa kutawala na kuwa na mamlaka juu ya yote, iwe dhambi, unyanyaso na nguvu zote za giza na shetani.
Utakaso wa mamlaka na utawala Maanake ni kwamba mahali ambapo wengine wanatawalwa na dhambi, utumwa na nguvu za shetani, sisi tulio wana wa utakaso na ahadi za Mungu tunapata ushindi na tumepewa mamlaka na ushindi kutawala kila hali.
Utawala si jambo la kuvumilia katika vita vya maisha, lakini ni haki ya kutawala juu ya kila hali.
Utawala wetu si kukimbia hali ya kushindwa katika kila sehemu ya maisha.
Somo na ujumbe wetu leo ni wa maana sana wakati huu, kwa maana watu wengi wanaishi chini ya utumwa na kunyanyaswa na hali ya maisha ki-uchawi, vita vya kiroho, shida za jamii na uzito wa dunia hii.
Biblia inatuhakikishia kwamba walio wa Yesu Kristo ni zaidi ya washindi. Agano la utakaso linahakikishia wewe kwamba, hautakufa mahali wengine watakufa, hautaishia mahali wengine wataishia, hii ni kwa sababu Mungu amekutakasa, amekuweka wakfu, amekutenga upate kutawala.
Hebu tuone:-
MPANGO WA KWANZA WA MUNGU ULIKUWA NI KUTAWALA NA KUMILIKI.
- Mungu alimuumba mwanadamu kutawala lakini si kutawaliwa.
- Utawala huo hukuwa mpango na wazo la mwanadamu bali mpango wa muumba vyote.
- Utawala ulikuwa tamko la Mungu. Utawala ulikuwa ni baraka ya Mungu kwa mwanadamu.
- Unapotembea katika imani ya kufahamu kwamba wewe ni mtawala, hapo utaanza kufahamu hali yako katika Agano la utakaso.
Utawala na mamlaka ni mpango wa Mungu-Mwanzo 1:26.
- Mungu alimpa mwanadamu utawala juu ya viumbe vyote. Huu ulikuwa mpango wa Mungu milele na milele.
- Mungu hataki tuishi mbali na mpango wake kwetu.
Utawala ni baraka, si kung’ang’ania-Mwanzo 1:28.
- Utawala ni baraka kutoka kwa Mungu. Mungu alimpa mwanadamu mamlaka na utawala ikiwa mwanadamu ataishi katika utii.
Maanake utawala ni mamlaka na kumiliki-Zaburi 8:6.
- Tumepewa mamlaka, tumetawazwa juu ya kazi za mikono yake.
- Mungu amevitia vitu vyote chini ya miguu yetu.
- Hivyo ni lazima kutumia mamlaka juu ya dunia yako-mazingira yako yote.
Utawala unakutakasa kutokana na utumwa na unyanyaso-Luka 10:19.
- Kristo amekuokoa na kukutakasa kutoka hali ya kunyanyaswa, amekupa nguvu na mamlaka juu ya nguvu zote za shetani na giza.
- Mungu alimtakasa Yusufu kule Misri kutokana na vikwazo, akampandisha juu zaidi, akatawala Misri yote-Mwanzo 41:39-44.
DAMU YA YESU KRISTO NDIYO MSINGI WA UTAWALA NA MAMLAKA.
- Damu ya Yesu Kristo ni mhuri wa Agano la utakaso.
- Agano la utakaso katika damu ya Yesu Kristo inawaondoa waliookoka kutoka uaribifu na kuwaweka mahali pa utawala.
- Pasipo damu ya Yesu Kristo mwanadamu anakaa chini ya hukumu-lakini panapo ile damu utawala unapatikana.
Damu ya Kristo inatupa ushindi juu ya adui-Ufunuo 12:11.
- Wakristo wanashinda shetani, si kwa nguvu zao, lakini kwa damu ya mwana kondoo na neno la ushindi wao.
Damu ya Kristo inashinda mashtaka yote ya adui-Wakolosai 2:14.
- Chochote kinacho kushtaki kinashindwa na damu ya Agano la utakaso.
Damu ya Yesu Kristo inakutakasa na hukumu na uaribifu wote-Kutoka 12:3.
- Misri ilipopata ghadhabu, wana wa Israeli walipata kupona kupitia ile damu ya mwana kondoo.
Damu ya Yesu Kristo imetufanya Wafalme na makuhani-Ufunuo 5:10.
- Kupitia damu ya Yesu Kristo tunatawala duniani na mamlaka yote.
UTAWALA NA MAMLAKA JUU YA DHAMBI NA TAMAA ZA MWILI.
- Utawala kamili si juu ya mambo ya nje tu lakini pia mambo ya ndani na vita vya kiroho.
- Dhambi ni mwizi mkuu wa mamlaka.
- Lakini ndani ya Yesu Kristo, nguvu za dhambi na tamaa za mwili, zimeshindwa.
Dhambi haina nguvu juu yako-Warumi 6:14.
- Neema ya Mungu inakufanya kuishi juu ya dhambi na kutembea katika haki.
Roho Mtakatifu anatupa nguvu-Wagalatia 5:16.
- Kwa kutembea katika Roho umetakaswa kutoka kutimiza tamaa za mwili.
Utawala na mamlaka zinahitaji nidhamu na utakatifu-1 Wakorintho 9:27.
- Kiasi na utakatifu vinatudumisha katika mamlaka ndani ya Yesu Kristo.
Utawala unadumishwa kupitia utakaso-2 Timotheo 2:21.
- Chombo kitakatifu ndicho Mungu anatumia.
- Danieli alijitakasa ndiposa Mungu akamtumia zaidi.
- Danieli alikaa katika utawala na mamlaka, Babeli na Persia.
- Danieli alielewa sana utawala na mamlaka-Danieli 6:3-4.
MAMLAKA JUU YA NGUVU NA FALME ZA GIZA.
- Nguvu za giza na falme za shetani zinatafuta sana kudhibiti wanadamu. Lakini Wakristo wamepewa utakaso na nguvu za kushinda katika Yesu Kristo.
- Utawala na mamlaka Maanake ni kwamba hatuko chini ya uwezo wao kwa maana mamlaka yetu yako juu zaidi kuliko yao.
Yesu Kristo alizivua enzi na mamlaka-Wakolosai 2:15.
- Kupitia kifo na kufufuka kwa Yesu Kristo. Yesu Kristo alivunja mipango yote ya shetani, huku akitupatia ushindi.
Utawala na mamlaka ni maisha ya ushindi katika vita vya kiroho-Waefeso 6:12.
- Hata ingawa vita viko, lakini tumewekwa ndani ya Kristo, tupate ushindi kila mara.
Utawala na mamlaka yanapatikana kupitia maombi-Luka 18:1.
- Maombi itakufanya kuwa katika ushindi kila mara.
Utawala na mamlaka yanapatikana katika maombi-Mathayo 4:4.
- Paulo na Sila walionyesha ushindi wao kwa maombi na sifa katika lile gereza.
MWISHO
- Kutakaswa kwa mamlaka na utawala Maanake ni kuishi juu ya vikwazo, vidhibiti, utumwa na kushindwa kunao angamiza watu wengine.
- Tembea katika ukweli wa utawala na mamlaka uliyopewa.
- Kataa kuishi chini ya utumwa wa dhambi, hofu na nguvu za shetani.
- Kupitia nguvu za Roho Mtakatifu, neno la Mungu, damu ya Yesu Kristo umepewa utawala katika kila sehemu ya maisha yako, kiroho, kimwili, kifedha na kiumma.
Latest posts by Rev, DR. Willy Mutiso (see all)
- CHRISTMAS: THE BIRTH THAT BROKE EVERY BONDAGE - December 25, 2025
- CHRISTMAS: WHY DID CHRIST COME? - December 24, 2025
- KRISMASI MAANAKE NI FURAHA KWA DUNIA YA DHIKI NA SHIDA - December 21, 2025
